Uchumi
Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 hadi 2020 umeainisha jukumu kubwa la nchi yetu katika kipindi hiki ni kutekeleza lengo la Dira 2025...

KUJENGA MSINGI WA UCHUMI WA KISASA WA TAIFA LINALOJITEGEMEA

Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 hadi 2020 umeainisha jukumu kubwa la nchi yetu katika kipindi hiki ni kutekeleza lengo la Dira 2025 la kuleta mapinduzi ya uchumi yatakayoitoa nchi kutoka kwenye dimbwi la uchumi ulio nyuma na tegemezi na kuiingiza katika mkondo wa uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea. Ili kufikia lengo hili Mwelekeo wa CCM unahimiza Serikali kutekeleza majukumu yafuatayo:-

  1. Kujenga Uchumi wa Kisasa wa Taifa Linalojitegemea, yaani modenaizesheni ya uchumi
  2. Kutekeleza Sera ya Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi
  3. Kutekeleza Sera ya Dola Kupanga Mipango na Kusimamia Uchumi
  4. Kuongeza uwezo wa Maarifa (sayansi na teknolojia) katika nchi kwa kutilia mkazo ubora wa Elimu na Raslimali Watu ya Nchi.
  5. Kuweka msingi wa miundombinu ya uchumi wa kisasa kwa kuhakikisha nishati yenye uhakika na uboreshaji wa miundombinu na huduma za kiuchumi kwa jumla.
  6. Kutumia fursa za kijiografia katika kukuza uchumi wa kisasa wa nchi.
  7. Kuhimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kufanya kazi
  8. Kuhakikisha uwiano wa mapato ili kujenga amani katika nchi na utulivu wa uchumi na maendeleo
  9. Kuweka methodolojia ya kusimamia utekelezaji wa majukumu haya ili kuhakikisha yanafanikiwa

Changamoto za kuibadili nchi yetu kutoka uchumi ulio nyuma na tegemezi kuelekea kwenye uchumi wa kisasa wa taifa linalojitegemea ni nyingi. Uzoefu wa utekelezaji tulioupata katika kipindi cha Mwelekeo wa Miaka 2000 hadi 2010 na kipindi cha Ilani ya Uchaguzi ya 2005 hadi 2010 cha Awamu ya Nne unaonyesha kuwa jukumu hili linapaswa liendelezwe katika kipindi cha Ilani hii kwa kuzingatia:

  1. Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025
  2. Dira ya Maendeleo Zanzibar 2020
  3. Malengo ya Milenia
  4. Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania, (MKUKUTA)
  5. Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA)
  6. Kilimo Kwanza

Ilani hii ya 2010-2015 inalenga kuongeza kasi ya utekelezaji wa mchakato wa kujenga uchumi wa kisasa na taifa linalojitegemea kwa kuwashirikisha na kuwawezesha kiuchumi wananchi.

Dhana ya Kujenga Uchumi wa Kisasa inalenga katika modenaizesheni ya uchumi. Modenaizesheni kimsingi ni kuongeza maarifa na matumizi ya sayansi na teknolojia katika sekta za uzalishaji. Modenaizesheni ya uchumi inalenga katikakuongeza uzalishaji, ufanisi na tija katika uchumi hususan katika kilimo,ufugaji, uvuvi na viwanda.

Mapinduzi ya kilimo ni msingi wa ukombozi wa uchumi wa nchi yetu. Katika kipindi cha Ilani hii 2010-2015 utekelezaji utaelekezwa katika modenaizesheni ya kilimo kwa kutilia mkazo Programu ya Kilimo Kwanza, upatikanaji fedha za uwekezaji katika sekta ya kilimo, mbegu bora, zana za kisasa,matumizi ya mbolea, elimu kwa wakulima kuhusu kanuni za kilimo, huduma za ugani, mikopo kwa wakulima, upatikanaji wa masoko, utafiti na matokeo, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Kufikiwa kwa lengo hili kutategemea sana mchango wa Serikali katika kusimamia mikakati ya kusimamia mapinduzi ya kilimo, ya kuunda Benki ya Kilimo na kutoa msukumo wa kimaeneo, kimkoa na kikanda katika mazao, uwekezaji na masoko.

Ufugaji ni moja ya sekta zinazohitaji kusimamiwa ili iweze kuchangia ipasavyo katika uchumi wa kisasa. Katika kipindi cha Ilani 2010-2015 mkazo utaelekezwa katika matumizi ya maarifa katika sekta ya mifugo. Jukumu kuu la msingi katika ufugaji litakuwa ni kuleta mabadiliko yatakayoiondoa sekta hii kutoa uduni wa ufugaji na kuwabadili wafugaji wetu kutoka wafugaji wahamaji. Mkazo utaelekezwa katika kutatua matatizo ya malisho na maji na kuwafikisha wafugaji katika ukulima mchanganyiko na ufugaji wa mabandani wenye tija kubwa, utakaotoa nyama na maziwa bora.

Uvuvi ni moja ya sekta za uchumi ambazo hazijapatiwa msukumo wa kutosha. Modenaizesheni katika uvuvi italenga katika kuwapatia maarifa wavuvi yatakayobadili na kuongeza uzalishaji wa samaki. Kuongeza ufanisi na tija na kubadili maisha ya wavuvi ni moja ya mapinduzi yanayolengwa katika Ilani ya 2010-2015. Katika kutekeleza hili Serikali itatilia mkazo uwezeshaji wa wavuvi, kuendeleza viwanda vya samaki, kusimamia uvunaji endelevu wa samaki katika bahari kuu.

Modenaizesheni ya uchumi itazingatia umuhimu wa viwanda kuwa ni kiongozi wa uchumi wa kisasa. Katika kuzingatia ukweli huu Ilani hii ya 2010-2015 itatekeleza dhana hiyo kutoa msukumo katika mapinduzi ya viwanda, kuhamasisha maendeleo ya sayansi, teknolojia na uhandisi, viwanda vya msingi, viwanda vya kati na viwanda vidogo.

Ufikiaji wa lengo letu kla ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea utategemea sana ushiriki wa wananchi wetu kupitia Sera ya Chama ya Uwezeshaji Wananchi. Sera hii itatekelezwa na kuimarishwa katika kipindi cha Ilani hii kwa Serikali kuendeleza yafuatayo:

  1. Mkakati wa MKURABITA
  2. Ushirika
  3. Mifuko ya Uwezeshaji:-
  4. Mfuko wa Wajasiriamali Wadogo
  5. Mfuko wa Mikopo Makampuni ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SMEs)
  6. Mfuko wa Pembejeo za Kilimo
  7. Mfuko wa Maendeleo ya Jamii
  8. Benki ya Wanawake

Aidha Sera ya Uwezeshaji itapewa msukumo mkubwa ili Watanzania waweze kuwezeshwa kushindana katika uchumi wa dunia na ule wa kanda.

Nchi yetu inahitaji uchumi imara na unaokua kwa kasi kubwa na endelevu ili kutatua tatizo letu la umaskini na utegemezi. Ni mapinduzi ya kilimo na viwanda ndiyo yatakayotuhakikishia kufika katika lengo hilo na nchi yetu kuwa na uchumi wa kati.

Comments are closed.