Katika kipindi cha Ilani hii, Chama Cha Mapinduzi kitaitaka Serikali ielekeze nguvu zake katika kuhifadhi, kulinda, kuendeleza, kudumisha, kuboresha na kuvuna maliasili ya wanyamapori, misitu na nyuki kwa manufaa ya Taifa kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
- Kuongeza msukumo katika kuendeleza ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kuzalisha asali na nta kibiashara.
- Kuweka utaratibu shirikishi wa upandaji miti, uvunaji na udhibiti wa moto. Ushirikishaji huo utakuwa wa sekta binafsi, NGOs na vijiji.
- Kuwezesha jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kunufaika na rasilimali za wanyamapori na misitu.
- Kuboresha miundombinu ndani ya mapori ya akiba, hifadhi za wanyamapori na misitu.
- Kuendelea kuboresha mazingira ya makazi ya watumishi wanaoishi katika mazingira magumu.
Utalii
Katika kipindi cha utekelezaji wa Ilani hii, Chama kitaielekeza Serikali iendelee kuitangaza hazina ya utalii tuliyonayo kwa mbinu za kisasa ili kukuza zaidi mchango wa utalii kwa pato la Taifa kwa kutekeleza yafuatayo:-
- Kujenga Chuo Cha Utalii ili kuimarisha mafunzo ya hoteli na utalii kwa lengo la kuongeza wingi na ubora wa watumishi wa huduma hizo.
- Kukuza mwamko na kuendesha kampeni za kuwashawishi Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii.
- Kupanua wigo wa aina za utalii kwa kuendeleza utalii wenye kuhusisha utamaduni, mazingira, makumbusho (historia) na michezo kama vile golfu.
- Kujihusisha kwa ukamilifu katika kutangaza fursa za kitalii zilizomo nchini na kuongeza bajeti ya kutangaza utalii ifanane na zile za nchi jirani.
- Kufanya juhudi maalumu za kutafuta masoko mapya ya utalii katika nchi zinazoinukia kiuchumi kama vile China na nchi nyingine za Asia.
- Kuandaa mikakati ya kuziba mianya ya uvujaji wa mapato ya utalii.
- Kuhimiza wawekezaji wa ndani na nje kujenga hoteli za kitalii za hadhi ya nyota 3 hadi 5.
- Kuzitathmini hoteli zilizopo na kuzipanga katika madaraja ya nyota zinayostahili. Wakati huo huo kuhakikisha kuwa hoteli zinakuwa katika hali ya unadhifu.
- Kuendeleza jitihada za kuhifadhi mazingira katika mbuga za wanyama, misitu fukwe, za bahari na maziwa.
- Kuwavutia watalii wa nje kwa kuboresha huduma na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora kwa kutumia teknolojia rahisi na za kisasa ili ziwavutie watalii.
- Kuhakikisha kuwa kuna usafiri wa uhakika wa ndege ili kuimarisha utalii.

