Kilimo
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya utekelezaji wa Ilani ya 2010-2015, Chama kitazielekeza Serikali kutekeleza kwa ukamilifu malengo ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) pamoja na kaulimbiu ya Kilimo Kwanza inayotoa msukumo katika kutekeleza mambo mbalimbali.

Mapinduzi ya Kilimo Kilimo ndio msingi wa uchumi wa kisasa na njia sahihi ya kuutokomeza umasikini.

Chama Cha Mapinduzi kinaamini kwa dhati kwamba kilimo cha kisasa kinachotumia Kanuni na zana bora za kilimo ndio ufunguo wa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu. Kilimo cha kisasa kina uwezo wa kutoa mazao mengi zaidi kutoka kila ekari iliyolimwa. Kwa nchi yetu, ziada hiyo ya mazao ina faida kubwa zifuatazo:-

  1. Kuipatia kila familia, kijiji na Taifa chakula cha kutosha ili kukomesha njaa.
  2. Kulipatia Taifa mavuno mengi ya kuuza ili kupata fedha za kigeni kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
  3. Ziada ya mazao huunda mazingira muafaka ya kuanzishwa viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani.
  4. Familia yenye ziada ya mazao huutokomeza umaskini kwa kuuza ziada hiyo kwenye soko na kupata fedha za kujiletea maendeleo.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya utekelezaji wa Ilani ya mwaka 2005-2010,  Serikali zetu zilichukua hatua kubwa katika kukipatia kilimo mwelekeo wa kisasa ili kiondokane na zana duni, mashamba madogo, kutozingatia kanuni bora za kilimo na kuridhika na mavuno ya kujikimu.

Katika kipindi cha miaka mitano ijayo ya utekelezaji wa Ilani ya 2010-2015, Chama kitazielekeza Serikali kutekeleza kwa ukamilifu malengo ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (ASDP) pamoja na kaulimbiu ya Kilimo Kwanza inayotoa msukumo katika kutekeleza mambo yafuatayo:-

  1. Kuanzisha Benki ya Kilimo yenye uwezo mkubwa ili ianze kuwakopesha wakulima wakubwa na wadogo kwa masharti nafuu.
  2. Kutumia uongozi shirikishi katika kusimamia kilimo na kuwafikishia wakulima vijijini maarifa yanayohusu kanuni za kilimo bora cha mazao wanayolima.
  3. Kuziweka tayari Benki Kuu na Hazina kukipatia kilimo chetu fedha za kutosha kwa kuhakikisha kwamba Bajeti ya Serikali haiwi kizuizi cha maendeleo ya kilimo nchini.
  4. Kuongeza upatikanaji na utumiaji wa pembejeo za kilimo, hususan mbolea, mbegu na miche bora na kuweka mfumo utakaohakikisha upatikanaji wa pembejeo hizo kwa wakulima.
  5. Kuongeza upatikanaji na matumizi ya zana za kilimo kwa kuishirikisha sekta binafsi, kuhamasisha na kuwezesha vikundi vya wakulima, hususan vijana kupata mikopo ya pembejeo na zana za kilimo kutoka kwenye Mfuko wa Pembejeo.
  6. Kuimarisha mashamba ya mbegu ya serikali ili kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mazao ya nafaka, mikunde na mbegu za mafuta na kuzisambaza kwa walengwa ili wazitumie.
  7. Kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya kilimo ya aina zote, hususan mazao makuu ya biashara, mazao ya chakula, mboga na matunda, mbegu za mafuta na muhogo ili mavuno makubwa ya kila zao yapatikane ifikapo mwaka 2015 kwa viwango vinavyopimika.
  8. Kuweka msukumo mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji maji katika maeneo stahiki ili kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2015 karibu asilimia 25 ya mahitaji yetu ya chakula inapatikana kwa njia ya kilimo hicho.
  9. Kuimarisha huduma za ugani kwa kuongeza kasi ya kufundisha na kuajiri wataalam wa fani mbalimbali hasa wenye vyeti vya kilimo na kuwaeneza wanakohitajika hasa vijijini na kuwajengea mazingira mazuri ya kazi.
  10. Kuimarisha huduma za udhibiti wa visumbufu na magonjwa ya mimea kwa kujenga uwezo wa kudhibiti visumbufu vya mazao mara vinapojitokeza ili kumwezesha mkulima kupunguza upotevu wa mazao kabla na baada ya mavuno.
  11. Kuhamasisha ujenzi na matumizi ya maghala bora ya kuhifadhia mazao na kutoa mafunzo juu ya teknolojia sahihi za hifadhi bora kwa lengo la kupunguza upotevu wa chakula. Mpango mkakati uandaliwe wa kupanua hifadhi ya mazao ya chakula katika maeneo ya nchi ambako mazao ya chakula yanalimwa kwa wingi.
  12. Kuimarisha usindikaji wa mazao mbalimbali katika ngazi ya kaya ili kuongeza thamani na muda wa matumizi na upatikanaji wa chakula kwa ujumla.
  13. Kupima maeneo ya kilimo na mashamba ya wakulima wapate hati miliki na kuhimiza matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migogoro ya kijamii kama vile kati ya wazalishaji wa mazao na wafugaji.
  14. Kusimamia utaratibu wa mashindano ya kilimo kinachozingatia kanuni bora za kilimo kati ya vijiji, kata, tarafa, wilaya na mikoa.
  15. Kuimarisha uongozi wa Vyama vya Ushirika na kuvijengea uwezo kujiendesha kwa ufanisi.
  16. Kuimarisha shughuli za ukaguzi na usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini.
  17. Kuweka kanda zinazoeleweka za mazao ya chakula na ya biashara kwa kuzingita hali ya hewa na uzoefu uliopo. Mazao yanayohusika yalimwe kwa wingi katika kanda hizo.
  18. Kuwezesha Halmashauri 133 kununua vitendea kazi kwa wataalamu ifikapo mwaka 2015.
  19. Kuzalisha mbolea kwa wingi kwa ajili ya mapinduzi ya kilimo tunayoyafanya na kuhamasisha makampuni ya mbolea ili yaingize mbolea kwa wingi kukidhi mahitaji ya tani 385,000 ifikapo mwaka 2015.

Comments are closed.