Serikali itachukua hatua za kuboresha, kuimarisha na hata kupanua elimu ya Awali hadi ya Chuo Kikuu na kuhakikisha kwamba elimu ya ngazi zote itakayotolewa nchini tangu sasa iwe ya ubora utakaowawezesha vijana wetu kuchukua nafasi zao stahiki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla. Hivyo, lengo hilo litafikiwa kwa kuishirikisha sekta binafsi kwa ukamilifu katika kutekeleza yafuatayo:-
(a) Elimu ya Awali
- Kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi ina darasa la Elimu ya Awali lenye madawati yanayolingana na hali ya watoto wa elimu hiyo.
- Kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wa Elimu ya Awali ili wasiingiliane na wale wa shule za msingi.
- Kuandaa walimu wengi wa Elimu ya Awali na kuwapanga katika shule zinazohusika.
(b) Elimu ya Msingi
Kusimamia kwa ukamilifu utekekezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi awamu ya pili (MMEM II – 2007 – 2011) na kuandaa na kutekeleza awamu ya tatu (MMEM III):-
- Kununua na kusambaza vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule zote.
- Kuimarisha Vituo vya Walimu (Teacher Resource Centres) katika Kanda na Halmashauri zote ili viweze kutoa mafunzo ya walimu kazini.
- Kuimarisha utoaji wa mafunzo kwa walimu wa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi.
- Kuendelea kuweka msukumo katika uandikishaji wa watoto wote wa rika lengwa katika ngazi ya Elimu ya Msingi kufikia asilimia 100 mwaka 2015.
- Kuinua kiwango cha uandikishaji wa watoto wenye ulemavu na wenye mahitaji maalumu.
- Kuendelea kuratibu na kusimamia upatikanaji wa maslahi ya walimu wa shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu na kuyaboresha ili kuhakikisha kwamba mishahara itolewayo inazingatia hali halisi ya maisha na ya soko.
- Kuendelea kuimarisha ukaguzi wa shule na kuhakikisha kuwa kila shule inakaguliwa angalau mara moja kwa mwaka na taarifa za ukaguzi kufanyiwa kazi.
- Kuhakikisha kwamba kila shule ya msingi ina walimu, madawati, vitabu vya kiada kwa kila somo vya kutosha. Uwiano wa mwalimu mmoja kwa kila wanafunzi 60 ufanyiwe kazi.
- Serikali Kuu ihakikishe kwamba kila Manispaa au Halmashauri ya Wilaya inajenga vyoo vya kisasa na vya kutosha katika shule zote za msingi ambazo ziko chini yake. Sekta binafsi ishirikishwe katika utekelezaji wa mradi huu.
- Kuanzisha mradi kabambe wa ujenzi wa nyumba nyingi za walimu wa shule za msingi za vijijini kwa kuwashirikisha wadau wote. Utekelezaji uanzie katika Wilaya ambazo zina uhaba mkubwa wa nyumba za walimu.
- Kuongeza idadi ya wanafunzi watakaochaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2015.
- Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.
(c) Elimu ya Sekondari
Kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari awamu ya pili (MMES II – 2010 – 2014), kuandaa na kutekeleza awamu ya tatu (MMES III):-
- Kuendelea kutekeleza azma ya kuwa na angalau shule moja ya kidato cha tano na sita kwa kila tarafa.
- Kuongeza idadi ya wanafunzi wa kidato cha 4 kwenda kidato cha 5 kufikia asilimia 50 ya watoto wanaofaulu ifikapo mwaka 2015.
- Kuendeleza na Kuimarisha mafanikio tuliyofikia katika ujenzi wa shule za sekondari kwa kuongeza idadi ya walimu, kununua vifaa vya maabara, vitabu, kuimarisha Maktaba na kukabiliana na jambo lolote litakalopunguza ufanisi wa kiwango cha elimu katika shule hizo.
- Kuendelea kutekeleza mpango wa kujenga maabara ya Sayansi na ya Lugha katika kila Shule ya Sekondari ili kuboresha ufundishaji.
- Kuendelea kutekeleza Programu ya kufundishia na kujifunzia kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Shule za Sekondari. Kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Lugha na kuinua ufaulu wa masomo hayo.
- Kuendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba za walimu hasa sehemu za vijijini na maeneo magumu kufikika.
- Kuendelea kusimamia na kuimarisha michezo shuleni.
- Kupitia na kuimarisha mitaala ya elimu ya sekondari kulingana na mahitaji.
- Kusimamia ubora wa miundombinu ya shule za sekondari ili kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu.
- Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.
- Kurudisha utaratibu wa kuzipelekea shule vitabu na vifaa ili kuhakikisha kwamba shule hazitofautiani katika upatikanaji na utumiaji wa vifaa hivyo.
- Kuimarisha na kuboresha kwa kiwango kikubwa shule za vijana wenye vipaji maalumu ili lengo la kuzianzisha liweze kufikiwa kama lilivyokusudiwa tangu mwanzo.
- Katika shule za sekondari, uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 uzingatiwe kama hatua ya kuinua ubora wa elimu hiyo.
(d) Elimu ya Ualimu
Kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa Mkakati wa Maendeleo na Menejimenti ya Ualimu (Teacher Development Management Strategy – TDMS) katika utoaji wa mafunzo ya ualimu:-
- Kuanzisha mafunzo ya walimu wa shule za msingi watakaoandaliwa kufundisha masomo mawili tu ambayo kila mmoja anayamudu ili kuinua ubora wa elimu ya msingi.
- Kuandaa na kuendeleza walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi, Hisabati na Lugha katika Shule za Msingi na Sekondari.
- Kuongeza udahili wa wanachuo katika mafunzo ya Ualimu tarajali ngazi ya Cheti na Stashahada.
- Kutoa mafunzo kwa walimu kazini ili kuimarisha na kuendeleza mbinu za ufundishaji kwa walimu.
- Kutoa mafunzo ya TEKNOHAMA katika kufundishia na kujifunzia katika Vyuo vya Ualimu.
- Kuendelea kusimamia na kuimarisha michezo katika vyuo vya ualimu.
- Kuimarisha miundombinu ya vyuo vya ualimu ili kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu.
- Kuboresha maabara ya vyuo vya ualimu vyenye mchepuo wa sayansi na kuvipatia vifaa na kemikali zinazotakiwa kwa ajili ya mafunzo ya vitendo katika vyuo hivyo.
- Kuandaa mitaala wa mafunzo yatakayojumuisha masomo ya mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda ili kupata wataalamu wa kufundisha masomo hayo. Uandishi wa vitabu vya masomo hayo yaende sambamba na maandalizi ya mtaala huo.
- Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.
(e) Elimu ya Juu
Kusimamia kwa ukamilifu utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Juu:-
- Kuboresha utaratibu wa utoaji na urejeshwaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu.
- Kupanua wigo wa utoaji wa mikopo ili kila mwanafunzi aliye na sifa ya kuingia chuo kikuu apate mkopo.
- Kukarabati, kupanua na kuimarisha miundombinu ya vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki ili iweze kuhimili ongezeko kubwa la wanafunzi watakaomaliza elimu ya sekondari.
- Kuongeza udahili wa wanafunzi kwenye vyuo vya elimu ya juu Kuongeza idadi ya wanafunzi wa kike vyuo vikuu ili ifikie angalau asilimia 40 ya wanavyuo wanaodahiliwa kila mwaka.
- Kuandaa wahadhiri wa kutosha na wenye sifa za kufundisha kwenye vyuo vya elimu ya juu.
- Kuunganisha vyuo vikuu na taasisi za utafiti kwenye mtandao ili kuimarisha utafiti wa pamoja, kupanua elimu kiwango cha uzamili na uzamivu.
- Kuratibu na kusimamia utoaji wa Elimu ya Juu iliyo bora na kufanyika kwa utafiti ili ziweze kutatua matatizo ya kijamii na kiuchumi.
- Kuimarisha mazingira ya utoaji wa Elimu ya Juu na maslahi yanayoendana nayo ili wahadhiri wavutiwe kujiunga na kubaki katika vyuo vya Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu.
- Kuimarisha utoaji wa Elimu ya Juu kwa njia ya Masafa na Elimu Mtandao.
- Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.
(f) Mafunzo ya Ufundi
Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi:-
- Kuongeza kasi ya upanuzi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa kushirikisha sekta binafsi.
- Kuanzisha vyuo vya Ufundi Stadi angalau kimoja kwa kila wilaya ifikapo mwaka 2015.
- Kuendeleza mafunzo ya ufundi na kada za kati za fani mbalimbali.
- Kuongeza idadi ya wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi wenye sifa za kuendeleza progamu za elimu ya ufundi kuanzia ngazi ya ufundi sanifu hadi ngazi za juu.
- Kuendelea kuhamasisha wanafunzi wa kike kujiunga na Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
- Kuimarisha miundombinu ya Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
- Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.
(g) Elimu ya Watu Wazima Yenye Manufaa
- Kuandaa na kutekeleza mpango kabambe wa Elimu ya Watu Wazima Yenye Manufaa nchini kote.
- Kuimarisha Mipango ya Elimu ya kujiendeleza ikiwa ni pamoja na Elimu Masafa na Ana kwa Ana.
- Kuimarisha utoaji wa Elimu Nje ya Mfumo Rasmi kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) kwa kushirikiana na wadau wengine.
- Kuinua ubora wa utoaji elimu ya watu wazima kupitia Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (MUKEJA).
- Kuimarisha uwezo wa watendaji katika usimamizi na menejimenti ya programu za elimu katika ngazi zote.

