Afya
Maendeleo ya Taifa letu yataletwa na wananchi wenye afya bora inayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali. Katika miaka mitano ijayo.

Maendeleo ya Taifa letu yataletwa na wananchi wenye afya bora inayowawezesha kuzalisha mali na kutoa huduma mbalimbali. Katika miaka mitano ijayo, Serikali itatekeleza na Chama kutoa kipaumbele katika maeneo yaliyoainishwa katika MKUKUTA na Malengo ya Milenia kwa kutekeleza yafuatayo:-

(a) Kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), ambao unazingatia na kutoa kipaumbele katika maeneo yafuatayo:-

  • Upatikanaji wa rasilimaliwatu wenye ujuzi na wa kutosha katika Sekta ya Afya,
  • Uwepo wa miundombinu ya huduma za afya na ustawi wa jamii kwa kukarabati na kujenga vituo vya kutolea huduma katika Afya na Ustawi wa Jamii hasa ngazi ya kijiji na kata,
  • Kuongeza upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitenganishi katika vituo vya kutolea huduma; na
  • Kuimarisha mfumo wa rufaa toka ngazi ya kijiji hadi Taifa.

(b) Kuimarisha usafiri wa wagonjwa, vifaa vya huduma za afya na ustawi wa jamii, njia za mawasiliano ya simu, “redio call na Internet”, katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya na ustawi wa jamii, ili kuwezesha upatikanaji wa huduma za kawaida za dharura za rufaa, zilizo bora, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kuwawezesha watu wenye ulemavu kumudu maisha ya kila siku.

(c) Kuhakikisha vituo vyote vinapata dawa muhimu na vifaa vya teknolojia ya kisasa, ya kuchunguza na kutibu magonjwa ili kuboresha utoaji wa huduma za kinga, tiba na utengemao.

(d) Kuimarisha nyenzo, vifaa na Mfumo wa ufuatiliaji na ukaguzi wa Huduma za Afya na Ustawi wa Jamii, pamoja na upatikanaji wa Taarifa na takwimu za Uendeshaji ikiwemo ufanyaji tathmini na utafiti, wa huduma za Afya na Ustawi wa Jamii.

(e) Kuhakikisha kuwa, huduma za Bima ya Afya zinaboreshwa na kuungana na Mfumo wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na Tiba kwa Kadi (TIKA), ili ziwafikie Wananchi na kuongeza asilimia za wanachama kutoka 7.7 hadi 30 ifikapo mwaka 2015.

(f) Kuendeleza jitihada za kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma ya matibabu ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa matibabu hususan kwa maradhi ya moyo, figo, mishipa ya fahamu na saratani.

(g) Kuboresha huduma za Ustawi wa Jamii, Serikali inatarajia kufanya yafuatayo:-

  • Kutafsiri sheria 3 zifuatazo, Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009, Sheria ya usafirishaji Haramu wa Binadamu ya 2009 na Sheria ya Wenye Ulemavu ya 2010.
  • Kutengeneza kanuni za utekelezaji wa sheria hizo.
  • Kuhuisha miongozo iliyopitwa na wakati ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
  • Kufanya utambuzi wa watoto walio katika mazingira hatarishi katika wilaya 48 ambazo hazijafanya utambuzi.
  • Kupeleka huduma za ustawi wa jamii kwenye Halmashauri.
  • Kutoa mafunzo kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kwa ngazi za Shahada 30, Stashahada 20 na Udaktari 5.
  • Kununua magari kwa makazi ya wazee 10 na vyuo 4 vya ufundi kwa watu wenye ulemavu.
  • Kufufua vyuo 4 vya watu wenye ulemavu na kuvipatia rasilimali watu na fedha.
  • Kuboresha Chuo cha Walezi wa Kulelea Watoto mchana Kisangara na Ilonga ili kutoa Wataalamu ngazi ya Cheti na Diploma.
  • Kujenga vyuo 2 vya Ustawi wa Jamii na Jengo la Ofisi ya Ustawi wa Jamii.
  • Kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu kipya cha Udaktari pamoja na hospitali ya kufundishia katika eneo la Mloganzila, Dar es Salaam ambacho kitakuwa na kitivo cha matibabu ya moyo, saratani na mishipa ya fahamu. Aidha, katika Chuo Kikuu cha Dodoma kinajengwa Chuo kishiriki cha Udaktari.

(h) Kuimarisha huduma ya matibabu ya wazee nchini kwa kuwapatia vitambulisho na kuyatungia sheria matibabu yao ya bure ili waweze kutibiwa hivyo katika vituo vyote vya matibabu bila ya usumbufu wowote.

(i) Kuimarisha huduma za mama Wajawazito, Watoto Wachanga na Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ili kuendelea kupunguza idadi ya vifo vyao kwa kutoa mafunzo ya huduma ya uzazi wa dharura na kuimarisha huduma za “EMOs” katika vituo vyote vya afya nchini.

(j) Kuwajengea uwezo na kuimarisha ujuzi wa watumishi wa Sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii, katika ngazi zote za kutolea huduma.

(k) Kuvijengea uwezo vituo vinavyotoa huduma za afya na Ustawi wa Jamii nchini.

(l) Kuimarisha udhibiti wa magonjwa yanayoambukiza, yasiyoambukiza na yale  yaliyosahaulika.

Comments are closed.