Kilimo
Katika kipindi cha miaka mitano, Serikali iliendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005 ambayo ilibainisha wazi kuwa kilimo cha kisasa ndiyo msingi na sharti muhimu katika kujenga uchumi wa kisasa

Kilimo kimeendelea kukua kwa asilimia 5.1, kinachangia asilimia 25.7 katika Pato Ghafi la Taifa, kinachangia asilimia 95 ya chakula na kinatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 80 ya watanzania kutokana na kutekeleza kwa ufanisi Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (Agricultural Sector development Programme –ASDP) na Programu ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika (Cooperative Reform and Modernisation Programme –CRMP)

Matumizi ya pembejeo za kilimo yameongezeka kutokana na serikali kutoa ruzuku kwenye mbolea za viwandani, mbegu bora, miche bora na madawa. Kwa mfano mbolea yenye ruzuku imeongezeka kutoka tani 51,629 mwaka 2005/06 hadi tani 141,050 mwaka 2008/09. Katika mwaka 2009/2010 ruzuku ya pembejeo kwa mfumo wa vocha imelenga kuwanufaisha jumla ya wakulima 1,500,000 ikilinganishwa na wakulima 737,000 mwaka 2008/2009.

Huduma za ugani zimeendelea kuboreshwa kutokana na Wizara kuongeza idadi ya wataalam wa kilimo wanaohitimu kutoka katika vyuo vya kilimo na kuajiriwa kwa lengo la kutoa utaalam kwa wakulima vijijini. Kwa mfano, Idadi ya wanafunzi waliojiunga na vyuo vya kilimo nchini imeongezeka kutoka 1,460 mwaka 2007/2008 hadi 3,498 mwaka 2009/2010. Aidha idadi ya Wagani imeongezeka kutoka 3,379 mwaka 2007/2008 hadi 4,437 mwaka 2010.

Serikali imeendelea kuhamasisha matumizi ya zana bora za kilimo kama matrekta makubwa, matrekta madogo ya mkono (powertillers) na zana za kukokotwa na wanyamakazi. Kwa mfano jumla ya matrekta makubwa 472, matrekta madogo ya mkono (power tiller) 495 na majembe ya kukokotwa na wanyamakazi 62,194 yaliingizwa nchini na watu binafsi pamoja na makampuni kati ya mwaka 2008 – 2009.

Serikali ya Awamu ya Nne imefanikiwa kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula na hivyo kuhakikisha hakuna mwananchi anayekufa kwa njaa. Katika msimu wa 2006/2007 uzalishaji wa mazao ya chakula ulikuwa tani milioni 10.66 na mahitaji mwaka 2007/2008 tani milioni 10.03 na hivyo kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 106. Uzalishaji wa chakula katika msimu wa 2007/2008, ulikuwa tani milioni 10.78 na mahitaji ya mwaka 2008/2009, yalikuwa tani milioni 10.3 na Taifa lilijitosheleza kwa chakula kwa asilimia 104.  Msimu wa 2008/2009, uzalishaji ulifikia tani milioni 10.77 na mahitaji ya chakula mwaka 2009/2010 ni tani milioni 10.57 na Taifa lilijitosheleza kwa chakula kwa asilimia 102. Serikali imeendelea na utaratibu wake wa kugawa chakula katika maeneo yanayo kabiliwa na upungufu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi. Kwa mfano, mwaka 2009/2010 jumla ya tani 56,740 za mahindi zilisambazwa kwa wananchi wapatao 1,569,890.

Hali ya ushirika nchini imeendelea kuimarishwa chini ya utekelezaji wa Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika.Mfano Wanachama wa Vyama vya Ushirika wameongezeka maradufu kutoka wanachama 750,000 mwaka 2005 mpaka wanachama milioni 1.8 mwezi Mei 2009. Idadi ya Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS), imeongezeka kutoka vyama 1,875 mwezi Juni, 2005 hadi 5,330 mwezi Mei 2009 sawa na ongezeko la asilimia 184.3. Idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 291,368 hadi 819,492 katika kipindi hicho sawa na ongezeko la asilimia 181.3. Akiba na amana za wanachama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 85.6 hadi bilioni 145.0 sawa na ongezeko la asilimia 69.3. Mikopo iliyotolewa  kwa wanachama imeongezeka kutoka shilingi bilioni 65.7 hadi shilingi bilioni 380 sawa na ongezeko la asilimia 478.0

Comments are closed.