Mohammed Gharib Bilal ,mwanasayansi wa nuklia alizaliwa Unguja mwaka 1945 na kufanikiwa kumaliza elimu yake ya msingi katika skuli ya Makunduchi, wilaya ya Unguja mwaka 1958.
Elimu yake ya sekondari alipatia katika ya shule Beit-el-ras mwaka 1962 na kufanikiwa kuingia kidato cha tano mwaka 1963 katika skuli ya sekondari ya Lumumba, Zanzibar.
Kabla ya kumaliza kidato cha tano alipata scholarship ya kwenda Marekani,ambapo alisomea masomo ya fizikia katika Chuo Kikuu cha Howard na kuhitimu shahada yake ya kwanza katika fizikia na hesabati mwaka 1967.
Baada ya shahada ya kwanza alijiunga na Chuo kikuu cha Carlifonia kwa shahada ya juu kwenye Chuo cha Berkely na kupata shahada ya M.A Physics mwaka 1969. Baada ya kuhitimu alianza kazi kama msadizi wa elimu yaani, Teaching assistant
Mohammed Gharib Bilal alikuwa mkufunzi wa utafiti (research assistant) hadi mwaka 1976 alipofanikiwa kupata Phd ya fizikia kutoka Chuo Kikuu cha Carlifonia.
Baadae mwaka huohuo alijiiunga na Chuo kikuu cha Dar-es-salaam kama mhadhiri wa fizika katika kitengo cha fizikia.
Mwaka 1983 alichaguliwa kuwa mkuu wa Idara na kuongoza kitengo cha Fizikia ya Nyuklia.Katika kipindi hicho aliwafundisha zaidi ya wanafunzi 10 kwenye masomo ya shahada ya uzamili.
Mwaka 1983 alishiriki kuanzisha shirika la mionzi la Taifa kwa kuchangia kitaalamu maandalizi ya mswada ambao ulitupatia sheria ya udhibiti wa matumizi ya mionzi ya nyuklia nchini.
Mwaka 1988 aliteuliwa kuwa mkuu wa Kitivo cha Sayansi cha Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na kuendelea katika wadhifa huo hadi mwaka 1990 alipoteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara mpya ya wakati huo ya Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu mwaka 1990-1995.
Akiwa Katibu mkuu alishiriki katika kuanzisha utaratibu wa kuchangia gharama za elimu ya juu na kuanzisha utaratibu wa mikopo. Pia wizara hiyo ilianzisha Chuo Kikuu Huria , pamoja na kuanzisha udhibiti wa vyuo vya elimu ya juu ( accreditation council).
Mnamo mwaka 1988 Dr Bilal alianzisha mradi wa science camp mjini Zanzibar iliyolenga kuwahamasisha vijana kusoma sayansi na kuzisaidia shule za sekondari zote za Zanzibar(Unguja na Pemba) Kupata vifaa vya kuwezesha kufanya majaribio ya wanafunzi ili waelewe zaidi sayansi kwa vitendo.
Mradi huo hatimaye ulirithiwa na Wizara ya Elimu Zanzibar. Mradi huo uliwasisimua vijana wengi katika sayansi na kuwapa changamoto nyingi za kujifunza mada mbali mbali zilizogusa mazingira ya Zanzibar.
Akiwa mwalimu wa Chuo Kikuu Dr Bilal aliweza kushiriki katika bodi mbali mbali, kama vile Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH), Tume ya mionzi (NRC), Mwenyekiti wa science panel ya Inter university council of East Africa na pia alishiriki kuasisi masomo ya juu ya mazingira katika sayansi(1990).
Mohammed Gharib Bilal alipata fursa ya kuhudhuria semina na kozi fupi katika fani mbali mbali kwa mfano, semina za shirika la Atomiki (IAEA) 1980 Kwabena, Ghana. 1984/85. Fellowship chuo kikuu cha Singapore. Vilivile huudhuria vikao vya kila mwaka vya shirika la Atomic.
Mwaka 1995 Dr Mohammed Gharib Bilal aliteuliwa kuwa Waziri kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi 2000.
Na katika siasa Dr Bilali amekuwa akikitumikia Chama Cha Mapinduzi katika nafasi mbali mbali kama vile kuwa Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa na Kamati Kuu tangu mwaka 1995 na pia amekuwa Mlezi wa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Pwani.
Dr Bilal alikuwa Mwenyekiti wa kutafuta utaratibu bora wa kura za maoni wa kuwapata wagombea katika chaguzi za Dola kwa tiketi ya CCM.
Mwaka 2004, aliteuliwa na Chama kuwa Mwenyekiti wa Shirika la Magazeti ya Chama.
Mnamo mwaka 2007, Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe Jakaya Kikwete alimteua Dr Bilal kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Dodoma.

